UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55792-un_yatahadharisha_kuhusu_hali_mbaya_ya_wakimbizi_nchini_libya
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2019 03:26 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi nchini Libya

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi nchini Libya.

Shirika hilo la wakimbizi la kimataifa limesema katika taarifa yake ya jana Jumanne kwamba, kituo cha kukusanya na kuhamisha wakimbizi cha Umoja wa Mataifa mjini Tripoli hivi sasa kimejaa kupindukia, na hakina tena sehemu ya kuhifadhia wakimbizi. 

Kituo hicho kilianzishwa mwaka jana 2018 katika mji mkuu wa Libya, Tripoli kama sehemu ya kuwakusanya kwa muda na baadaye kuwapeleka sehemu nyingine wakimbizi hao.

Jenerali muasi Khalifa Haftar ana uhusiano wa karibu mno na watawala wa Saudi Arabia

 

Taarifa hiyo ya UNHCR imeongeza kuwa, baada ya kituo kilichokuwa kinatumika kama korokoro ya kuwashikilia wakimbizi kilichoko katika vitongoji vya Tripoli kushambuliwa kwa ndege za jenerali muasi Khalifa Haftar, tarehe 3 Julai mwaka huu na kupelekea wakimbizi 53 kuuawa, wakimbizi wengine 400 waliokuwepo kwenye viunga hivyo vya Tripoli wamepelekwa kwenye kituo hicho cha muda cha kuwahamishia wakimbizi maeneo mengine, na hivyo kusababisha msongamano mkubwa ndani ya kituo hicho.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu na taasisi za kimataifa nazo zimekuwa zikitahadharisha mara kwa mara kuhusu hali mbaya ya maelfu ya wakimbizi nchini Libya hasa baada ya jenerali muasi Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, mwezi Aprili mwaka huu.