Misri yataka kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Sudan
(last modified Tue, 10 Sep 2019 07:19:45 GMT )
Sep 10, 2019 07:19 UTC
  • Misri yataka kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Sudan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ametaka kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Sudan, akisisitiza kuwa serikali mpya ya kiraia ya Khartoum inahitaji uungaji mkono wa jamii ya kimataifa na sio kuendelea kuwekewa vikwazo na kutengwa.

Sameh Shoukry ambaye alikuwa afisa wa kwanza wa kigeni kuitembelea Sudan baada ya kuapishwa kwa serikali mpya ya kiraia nchini humo, alitoa mwito huo jana Jumatatu mjini Khartoum na kubainisha kuwa, "Kile ambacho Wasudan wamefikia ni jambo la kupigiwa mfano. Sudan hivi sasa inahitaji uungaji mkono kamili wa jamii ya kimataifa."

Siku ya Jumapili, serikali mpya iliapishwa nchini Sudan likiwa ni baraza la kwanza la mawaziri tangu Rais wa zamani wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir aondolewe madarakani Aprili mwaka huu.

Abdallah Hamdok, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan

Serikali ya Sudan imekuwa ikilaani vikali hatua ya serikali ya Marekani ya kuongeza muda wa vikwazo vyake dhidi ya nchi hiyo ya Kiafrika kila baada ya miezi kadhaa, licha ya kutolewa miito mbalimbali ya kuondoa kikamilifu vikwazo hivyo ambavyo Sudan iliwekewa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1993.

Washington iliiwekea Sudan vikwazo hivyo ikiituhumu kuwa inaunga mkono ugaidi.

Tags