Jeshi la Nigeria liliwazika Waislamu kwa umati wakiwa hai
Jeshi la Nigeria liliwaua mamia ya Waislamu nchini Nigeria na kuwazika katika kaburi la umati wakiwemo baadhi waliokuwa hai mwezi Desemba mwaka jana, imefichua Amnesty International.
Katika taarifa yake ya leo Ijumaa, Amnesty imesema jeshi la Nigeria liliua zaidi ya Waislamu 350 wanachama wa Harakati ya Kiislamu Nigeria inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky. Ripoti hiyo imefichua kuwa, jeshi la Nigeria lilijaribu kuficha ushahidi wa jinai hiyo kwa kuwazika mahanga katika makaburi ya umati huku watu wa kawaida wakizuiwa kufika katika baadhi ya maeneo ya jinai hiyo katika mji wa Zaria jimboni Kaduna.
Ikumbukwe kuwa Desemba 12 mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa katika kituo cha Kiislamu cha mji wa Zaria na kuwatuhumu kuwa walifunga njia ya msafara wa mkuu wa jeshi kwa njama ya kumuua.
Waislamu wa eneo hilo wamepinga vikali tuhuma hizo. Siku moja baadaye, jeshi la Nigeria lilivamia nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kumtia mbaroni sambamba na kuua mamia ya Waislamu waliokuwa wakimlinda. Katika matukio hayo mawili, mamia ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliuawa kwa umati, wakiwemo watoto wawili wa Sheikh Zakzaky. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa waliouawa katika tukio hilo ni zaidi ya elfu moja.
Amnesty International imesema jeshi la Nigeria liliwachoma moto Waislamu hai sambamba na kuteketeza nyumba na kuzika miili yao katika makaburi ya umati. Ripoti hiyo imesema si tu kuwa jeshi la Nigeria lilitumia nguvu ziada dhidi ya wanawake, watoto na wanaume na kisha kuwaua kwa umati, bali pia kumefanyika njama za makusudi za kuficha ukweli kuhusu jinai hiyo.
Amnesty International pia imeutaka utawala wa Rais Muhammadu Buhari kuchunguza muaji hayo ya Waislamu wasio na hatia.