Polisi Afrika Kusini: Kiwango cha mauaji nchini kinatisha
Polisi nchini Afrika Kusini imeeleza wasiwasi wake kutokana na kukithiri kwa kiwango cha mauaji ya kiholela nchini humo.
Bheki Cele, Waziri wa Polisi nchini humo alisema hayo jana Alkhamisi alipofika mbele ya Kamati ya Usalama ya Bunge la nchi hiyo na kuongeza kuwa, akthari vya mauji hayo yamefanyika miongoni mwa watu wa karibu wa familia, majirani na marafiki.
Amesema kutokana na ukweli huo, inakuwa vigumu kwa vyombo vya usalama kuweza kudhibiti mauaji ya aina hiyo. Waziri wa Polisi wa Afrika Kusini ametoa mwito kwa wanasaikolojia kuchunguza visa hivyo, na kuandaa ripoti itakayotoa maelezo ya kina na sababu za kuongezeka kwa mauaji ya namna hii.
Kwa mujibu wa takwimu za polisi huko Afrika Kusini, watu 21,022 waliuawa nchini humo kati ya Aprili 2018 na Machi 2019, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 1.4 ikilinginishwa na mauaji yaliyofanyika katika kipindi kama hicho kati ya mwaka 2017 na 2018.
Nukta ya kuogofya ni kuwa, watoto 1014 ni miongoni mwa wahanga wa mauaji hayo ya kiholela, yaliyofanywa na watu wa familia, majirani, marafiki na wapenzi.
Kamanda Mkuu wa Polisi nchini humo, Meja Jenerali Norman Sekhukhune amesema visa 736 kati ya 1014 vya mauaji ya watoto yalifanywa na watoto wenzao wenye chini ya umri wa miaka 18.