Watu 50 waaga dunia katika ajali ya treni Kongo DR
(last modified Fri, 13 Sep 2019 02:38:18 GMT )
Sep 13, 2019 02:38 UTC
  • Watu 50 waaga dunia katika ajali ya treni Kongo DR

Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya treni iliyotokea mapema jana Alkhamisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Steve Mbikayi, Waziri wa Masuala ya Kibinadamu wa nchi hiyo amesema ajali hiyo ilitokea alfajiri ya jana kabla ya kupambazuka, katika mji wa Mayibaridi mkoani Tanganyika, kusini mashariki mwa nchi.

Habari zaidi zinasema kuwa, garimoshi hilo la abiria liliacha reli alfajiri ya jana na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 50 huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Waziri wa Masuala ya Kibinadamu wa DRC amebainisha kuwa, idadi hiyo iliyotolewa na serikali ni ya muda, na yumkini ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata abiria. 

Wakongomani waliojazana kwenye treni ya uchukuzi wa umma

Mwezi Machi mwaka huu, ajali nyingine ya garimoshi la kusafirishia mizigo ilitokea katika mkoa wa Kasai wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kupelekea watu 50 kupoteza maisha huku wengine wapatao 80 wakijeruhiwa.

Ajali kubwa za treni zimekuwa zikitokea mara kwa mara huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni kuchakaa kwa reli, magarimoshi na mabehewa ambayo ni ya tangu enzi za ukoloni katika muongo wa 60.