Somalia yavunja majaribio mawili ya kutaka kumuua Waziri Mkuu wa nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56021-somalia_yavunja_majaribio_mawili_ya_kutaka_kumuua_waziri_mkuu_wa_nchi_hiyo
Waziri Mkuu wa Somalia ameokoka katika majaribio mawili ya kutaka kumuua, majaribio ambayo genge la kigaidi la al Shabab limetangaza kuhusika nayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2019 07:57 UTC
  • Somalia yavunja majaribio mawili ya kutaka kumuua Waziri Mkuu wa nchi hiyo

Waziri Mkuu wa Somalia ameokoka katika majaribio mawili ya kutaka kumuua, majaribio ambayo genge la kigaidi la al Shabab limetangaza kuhusika nayo.

Shirika la habari la Anadolu limewanukuu maafisa wa polisi wa jimbo la Shebelle la kusini magharibi mwa Somalia wakithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, guruneti moja limeripuka katika mji wa bandari wa Merca, wakati Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khayre alipokuwa anahutubia kundi kubwa la watu. Mtu mmoja ameuawa kwenye shambulio hilo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, watu wengine wawili wameuawa katika shambulio la roketi lilifanywa dakika chache tu baada ya kutokea mripuko wa kwanza wa guruneti.

Wanamgambo wa al Shabab waliouliwa na jeshi la serikali Somalia

Hakuna madhara yoyote aliyopata Waziri Mkuu huyo wa Somalia na ujumbe wake. Hata hivyo wamelazimika kukatisha ziara yao hiyo na kurudi mjini Mogadishu.

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab ambalo linaendesha pia mashambulizi ya kigaidi hata katika nchi nyingine kama vile Kenya, limetangaza kuhusika na shambulio hilo. 

Serikali ya Somalia na askari wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanaendesha operesheni za pamoja za kupambana na magaidi hao na hadi hivi sasa wamefanikiwa kuwafurusha wakufurishaji hao katika miji yote mikubwa ya Somalia.