Makumi wahofiwa kufa maji katika ajali ya kuzama boti Kongo DR
(last modified Mon, 16 Sep 2019 11:55:13 GMT )
Sep 16, 2019 11:55 UTC
  • Makumi wahofiwa kufa maji katika ajali ya kuzama boti Kongo DR

Makumi ya watu wanahofiwa kupoteza maisha katika ajali ya kuzama boti iliyotokea katika kijiji cha Mambutuka, eneo la Maluku huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Polisi ya DRC imethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa ajali hiyo imetokea katika Mto Congo viungani mwa mji mkuu Kinshasa, na kwamba boti hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya watu 100 kabla ya kuzama jana Jumapili.

Taarifa ya polisi ya nchi hiyo imesema hatima ya watu 36 waliokuweko kwenye boti hiyo haijulikani, na kwamba wapigambizi wa Jeshi la Majini la DRC wamefanikiwa kuwanusuru watu 76.

Duru za habari zinasema boti hiyo ilikuwa imejaa kupindukia, na kwamba ilikuwa inatokea mkoa wa Mai-Ndombe, kusini magharibi mwa Kinshasa, 

Boti iliyojaa kupita kiasi DRC

Mwezi uliopiota, watu wasiopungua 12 walipoteza maisha kufuatia ajali ya boti huko katika Mto Lukenye katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ikumbukwe kuwa mwezi Mei mwaka huu takriban watu 100 walipoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wameabiri kuzama katika Ziwa Kivu nchini DRC. Ajali kama hizo zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.