Mateka Muirani aachiwa huru na maharamia wa Somalia
Raia wa Iran ambaye amekuwa akishikiliwa mateka na maharamia wa Somalia kwa miaka kadhaa sasa hatimaye ameachiwa huru.
Shirika la kibinadamu la kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa na maharamia wa Somalia limesema katika taarifa ya jana Jumamosi kuwa, Mohammad Sharif Panahandeh ambaye hali yake ya afya imezorota amechiwa huru na atarejea nyumbani ndani ya siku chache zijazo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Panahandeh ni mmoja wa mateka wanne waliokuwa wanashikiliwa na maharamia wa Kisomali tokea Machi 2015.
Uharamia umepungua kwa kiasi kikubwa katika pwani ya Somalia katika miaka ya hivi karibuni kutokana na jitihada za nchi mbalimbali.
Hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Ubaharia (IMO) lilipongeza nafasi ya Iran katika kukabiliana na maharamia na kulinda usalama wa maji ya Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden.
IMO inasema manowari za Jeshi la Majini la Iran zinalinda doria sambamba na kusindikiza meli za mafuta na za kibiashara katika Ghuba ya Aden na Bahari ya Hindi.