UN: Mapigano yamefanya watu 40,000 wakimbie Nigeria
(last modified Sat, 28 Sep 2019 11:14:29 GMT )
Sep 28, 2019 11:14 UTC
  • UN: Mapigano yamefanya watu 40,000 wakimbie Nigeria

Umoja wa Mataifa umesema mapigano na ghasia huko kaskazini magharibi mwa Nigeria zimefanya makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wakimbilie usalama wao katika nchi jirani ya Niger.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema Wanigeria 40,000 eneo la kaskazini magharibi mwa nchi wamevuka mpaka na kuingia katika nchi jirani ya Niger, kutokana na kushadidi mashambulizi ya watu wanaobeba silaha na majambazi.

Msemaji wa UNHCR, Babar Baloch amesema taasisi hiyo ya UN haina taarifa yoyote kuhusu wahusika wa jinai hizo katika majimbo ya Sokoto, Zamfara and Katsina. Serikali ya Abuja imekuwa ikidai kuwa ukatili huo unafanywa na magenge ya wabeba silaha.

Duru za habari zimesema mauaji, mapigano, ubakaji na mashambulizi yanayofanywa katika maeneo hayo hayafanywi na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Wakimbizi wa Nigeria nchini Niger

Mapema mwezi huu, viongozi wa majimbo ya mpakani ya Niger na Nigeria walifanya vikao vya pamoja kwa madhumuni ya kukabiliana na vitendo vya mabavu vinavyotekelezwa na makundi ya wabeba silaha.

Tangu mwaka uliopita, Niger imeimarisha usalama katika mpaka wake na Nigeria kwa lengo la kukabiliana na  makundi ya wabeba silaha ambayo yamepelekea wimbi kubwa la raia wa Nigeria kuhamia katika eneo la Maradi.

Tags