Rais wa Kodivaa (78): Nina hamu ya kukabidhi madaraka kwa vijana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56326-rais_wa_kodivaa_(78)_nina_hamu_ya_kukabidhi_madaraka_kwa_vijana
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast amesema ana hamu kubwa ya kukabidhi madaraka kwa kizazi cha sasa cha vijana katika uchaguzi wa rais wa mwakani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 30, 2019 02:37 UTC
  • Rais wa Kodivaa (78): Nina hamu ya kukabidhi madaraka kwa vijana

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast amesema ana hamu kubwa ya kukabidhi madaraka kwa kizazi cha sasa cha vijana katika uchaguzi wa rais wa mwakani.

Rais Outarra mwenye umri wa miaka 78 amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Dimbokro, ingawaje hajaeleza iwapo atagombea urais katika uchaguzi huo wa mwaka ujao au la.

Katika matamshi hayo ya kutatanisha, Rais wa Kodivaa amebainisha kuwa, "Nina hamu kubwa ya kukabidhi madaraka kwa kizazi cha sasa. Asilimia 75 ya taifa hili inaundwa na vijana wenye umri usiozidi miaka 30. Kuna mpango wa kuifanyia katiba marekebisho ili tuwe na kikomo cha umri wa kugombea urais. Lakini hii isitafsiriwe kuwa sitokuwa mgombea (katika uchaguzi ujao)."

Mmoja wa wapinzani wakuu wa Outtara ni Henri Konan Bedie  mwenye umri wa miaka 85, ambaye mwaka jana alijiondoa kwenye muungano tawala baada ya Rais Outtara kusema kuwa katiba mpya iliyoidhinishwa mwaka 2016 inamruhusu kuwania muhula wa tatu. 

Wananchi wakipiga kura katika uchaguzi uliopita Kodivaa

Ouattara ambaye aliingia madarakani baada ya mgogoro wa umwagikaji damu wa miezi mitano kati ya mwaka 2010 na 2011, kwa sasa anahudumia muhula wa pili unaotazamiwa kufikia tamati mwaka 2020.

Katika mahojiano na jarida la Jeune Afrique mwaka jana, Rais wa Kodivaa alisema, "Katiba mpya inaniruhusu kugombea mihula miwili kuanzia mwaka 2020, lakini nitatangaza uamuzi wangu wa mwisho wakati huo ukifika, na kwa kutegemea mazingira yatakayokuwepo hapa nchini."