Amnesty International: Misri ni gereza kubwa la wakosoaji wa serikali
(last modified Mon, 30 Sep 2019 08:11:09 GMT )
Sep 30, 2019 08:11 UTC
  • Amnesty International: Misri ni gereza kubwa la wakosoaji wa serikali

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa vikali ukandamizaji na kamatakamata dhidi ya waandamanaji nchini Misri na kusisitiza kuwa nchi hiyo imegeuzwa kuwa gereza kubwa la wakosoaji.

Katika taarifa, Amnesty International imeitaka serikali ya Misri kuheshimu haki na uhuru wa kujieleza na kukusanyika. Taarifa hiyo imesema, "Misri ikomeshe hatua zake kandamizi dhidi ya waandamanaji."

Hii ni katika hali ambayo, vikosi vya usalama vimepelekwa katika miji muhimu ya nchi hiyo hususan ile ambayo imekuwa mstari wa mbele kwa maandamano dhidi ya Rais Abdul-Fattah al-Sisi kwa shabaha ya kuzima maandamano hayo.

Wananchi wa Misri wamekuwa wakiandamana katika siku za hivi karibuni kulalamikia matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii wanayokabiliana nayo na kutaka kuondoka madarakani Sisi.

Maafisa usalama nchini Misri wanatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya wananchi

Duru za habari zinaarifu kuwa, watu zaidi ya 2000 wametiwa mbaroni na maafisa usalama katika maandamano hayo.

Maandamano ya sasa ambayo ni nadra kushuhudiwa nchini humo katika utawala wa Sisi, yanafanyika baada ya kupita miaka 8 ya vuguvugu la harakati ya wananchi wa Misri lililopelekea kung'olewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

Tags