Wakimbizi wa Burundi waliopo Tanzania kuanza kurejea nyumbani Alhamisi hii
Burundi leo imetangaza kuwa kundi la kwanza la wakimbizi wa nchi hiyo walioko Tanzania watarejea nyumbani Alhamisi wiki hii. Wakimbizi hao watarejea Burundi kwa umati kama sehemu ya mpango ulioratibiwa na serikali za nchi mbili hizo.
Afisa wa serikali ya Burundi anayehusika na zoezi hilo Nestor Bimenyimana amesema kuwa wakimbizi karibu elfu moja wapo katika kundi la kwanza la wale wanaorejea Burundi. Amesema zoezi hilo linafanyika kwa khiari.
Mwezi Agosti mwaka huu Burundi na Tanzania zilikubaliana kwamba, zoezi la kuwarejesha Burundi wakimbizi wa nchi hiyo wapatao laki mbili waliopo Tanzania litaanza Oktoba Mosi. Hatua hiyo imeibua wasiwasi kwamba, kuna uwezekano baadhi ya Warundi waliokumbilia Tanzania kutokana na machafuko ya ndani wakarejeshwa nchini kwao kwa nguvu na bila ya khiari yao wenyewe.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania amesema kuhusiana na zoezi hilo kwamba, ni waziri pekee ndiye anayeweza kuzungumzia operesheni hiyo.
Mamia ya raia wa Burundi wameuawa kwenye ghasia na machafuko yaliyoigubika nchi hiyo tangu mwaka 2015 wakati Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu, hatua ambayo ilikuwa ni kinyume na katiba ya nchi hiyo. Kipindi hicho raia zaidi ya laki nne wa Burundi walikimbilia nchi za nje hasa katika nchi jirani za Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.