Watu 22 wauawa katika mapigano Amhara, Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56419-watu_22_wauawa_katika_mapigano_amhara_ethiopia
Mapigano baina ya askari wa serikali ya kieneo na kabila la wachache yamepelekea watu wasiopungua 22 kuuawa katika eneo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia katika kipindi cha siku tano zilizopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2019 10:35 UTC
  • Watu 22 wauawa katika mapigano Amhara, Ethiopia

Mapigano baina ya askari wa serikali ya kieneo na kabila la wachache yamepelekea watu wasiopungua 22 kuuawa katika eneo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia katika kipindi cha siku tano zilizopita.

Mapigano hayo yalihusisha askari wa kikosi maalumu cha utawala wa eneo hilo na wanamgambo wa kabila la Kimant ambalo linataka mamlaka ya kujitawala.

Taarifa zinasema machafuko mapya yaliibuka Ijumaa iliyopita baada basi ambalo lilikuwa linasafiri kutoka Metema kuelekea Gondar katika eneo hilo la Amhara kushambuliwa na wanamgambo wa Kimant. Raia 10 waliokuwa ndani ya basi hilo waliuawa.

Mapigano hayo ni pigo kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye sera zake za mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi zimepelekea kupata nguvu viongozi wa kikabila ambao wanazidi kujiimarisha.

Mwezi Juni, Mkuu wa Jeshi la Ethiopia Jenerali Seare Mekonnen na maafisa wengine watatu wa ngazi za juu waliuawa katika jaribio la kuipindua serikali ya jimbo la Amhara kaskazini mwa nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Serikali ya Abiy Ahmed inakabiliwa na mashinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika majimbo ya nchi hiyo, likiwemo jimbo la Amhara, ambalo limekuwa kitovu cha mapigano ya kikabila nchini Ethiopia. Mfumo wa utawala wa Ethiopia ni wa kifederali au majimbo na kila jimbo lina rais mwenye mamlaka ya ndani.

Watu takribani milioni 100 nchini Ethiopia wameanza kushuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa. Abiy Ahmed ambaye alichukua madaraka mwaka jana amewaachilia huru waandishi habari na wanaharakati wa kisiasa na kuondoa marufuku ya vyama vya kisiasa sambamba na kuwapandisha kizimbani maafisa wa serikali wanaotuhumiwa kukiuka haki za binadamu.