Oct 05, 2019 15:05 UTC
  • Rais wa zamani wa Benin: Saudia inawasaidia kifedha magaidi wa Boko Haram

Rais wa zamani wa Benin amefichua kuwa, utawala wa Aal Saud wa Saudi Arabia unawasaidia kifedha magaidi wa Boko Haram wanaoendesha vitendo vya kigaidi magharibi mwa bara la Afrika.

Shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kumnukuu Nicéphore Dieudonné Soglo akisema hayo na kuongeza kuwa, Saudi Arabia na Qatar zinalisaidia kifedha genge la kigaidi la Boko Haram ambalo linaendesha ugaidi na kumwaga damu za watu katika nchi kadhaa zinazopakana na Ziwa Chad.

Rais wa zamani wa Benin, Nicéphore Dieudonné Soglo

 

Soglo ambaye mwaka 1990 alikuwa Waziri Mkuu wa Benin hadi mwaka 1991 ambapo alianza kuwa rais wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika hadi mwaka 1996, amesema hayo pambizoni mwa kikao cha kuimarisha demokrasia kilichofanyika Niamey, mji mkuu wa Niger na kuliambia gazeti la The Cable la Nigeria kuwa, genge la kigaidi la Boko Haram linaungwa mkono kifedha na marafiki zetu wa Saudi Arabia na Qatar. Baadaye amehoji kwa kusema: Je, kwa kuzingatia hali hiyo, naweza kuwaita hao kuwa ni marafiki zetu?

Genge la kigaidi la Boko Haram liliundwa mwaka 2009 na kuanza kuendesha vitendo vya kigaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria kabla ya kupanua wigo wa ugaidi wake mwaka 2015 na kufika katika nchi zote zinazopakana na Ziwa Chad yaani Cameroon, Niger, Nigeria na Chad. 

Hadi hivi sasa zaidi ya watu 27 elfu wameshauwa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi katika eneo hilo tangu lilipojitokeza genge hilo la kigaidi mwaka 2009. 

Tags