UN kusaidia kutafuta ndege iliyoanguka DRC
Umoja wa Mataifa umejiunga na oparesheni ya kusaidia kutafuta ndege ya mizigo ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyopotea tangu Alhamisi ikiwa na watu wanane ndani yake.
Kikosi cha Kulinda Amani Cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kimetangaza kuwa kilitumia ndege mbili na helikopta moja Jumamosi kujaribu kutafuta ndege hiyo ya Antonov 72.
Ndege hiyo ya mizigo ilikuwa imebeba vifaa vilivyotumika katika safari ya Rais Felix Tshisekedi mjini Goma na ilitoweka baada ya kuondoka mjini humo kuelekea Kinshasa huku kukiwa na hali mbaya ya hewa. Ndege hiyo ilikuwa imebaba wafanyakazi wa ofisi ya Rais Tshisekedi na marubani wake wawili wametajwa kuwa raia wa Russia.
Wafuasi kadhaa wa Tshisekedi waliandamana Ijumaa wakiwatuhumu wafuasi wa rais wa zamani Joseph Kabila kuwa walihusika na ajali hiyo.
Pamoja na hayo ajali za ndege aina ya Antonov, ambazo hutumika kwa wingi DRC, huripotiwa mara kwa mara nchini humo.