Maporomoko ya ardhi yaua watu 22 kusini mwa Ethiopia
Maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa yameuwa watu 22 kusini mwa Ethiopia.
Takele Tesfu, afisa wa serikali katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hadi sasa wamefanikiwa kufukua miili 17 kati ya 22 iliyofukiwa kwenye mapomoko hayo. Amesema miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni watoto wadogo sita na wanawake tisa.
Amesema maporomoko hayo ya udongo yalitokea siku ya Jumapili katika wilaya yenye milima mingi ya Konta, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Amesema mvua kubwa zilinyesha kwa saa kumi mfululizo siku hiyo na kusababisha mafuriko makubwa na mapomoko ya ardhi. Afisa huyo wa serikali katika wilaya ya Konta amesema shughuli ya kutafuta maiti zaidi kwa kutumia mikono na mashine itaendelea hii leo.
Mwezi Machi mwaka 2017, karibu watu 50 waliuawa kwenye maporomoko ya taka kwenye eneo moja kubwa la kumwaga taka nje ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.