Watu milioni 7.8 Ethiopia wanahitaji misaada ya kibinadamu
Takriban watu milioni 7.8 nchini Ethiopia wameendelea kuhitaji misaada ya kibinadamu katika muda uliobaki wa mwaka huu.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu OCHA ambayo imesema dola bilioni 1.064 zinahitajika kukabiliana na hali hiyo.
Ripoti hiyo inasema serikali ya Ethiopia na wadau wengine wa mambo ya kibinadamu wamejitahidi kukabiliana na changamoto za ukame unaokabili sehemu za mashariki na mashariki kusini, mafuriko yaliyotokea katika baadhi ya maeneo nchini humo, na mahitaji ya kibinadamu kwa watu waliopoteza makazi, waliorudi na jamii za kuwapokea.
Kwa mujibu wa OCHA, Waethiopia milioni 7.9 wamepokea msaada wa kibinadamu kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.
Kwingineko, mamia ya watu waliandamana Jumatano katika mji mkuu wa Ethiopia kumpinga Waziri Mkuu Abiy Ahmed na hivyo kutia doa Tuzo ya Amani ya Nobel ambayo ameshinda mwaka huu. Waandamanaji wamesema waziri mkuu alikuwa anapanga kumtia mbaroni Jawar Mohammed, muasisi wa mtandano huru wa vyombo vya habari.