Chama tawala Botswana chashinda uchaguzi mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56844-chama_tawala_botswana_chashinda_uchaguzi_mkuu
Chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) kimeshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo baada ya kupata viti 29 vya Bunge ambavyo ni sawa na asilimia 51 ya kura.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 25, 2019 06:37 UTC
  • Chama tawala Botswana chashinda uchaguzi mkuu

Chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) kimeshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo baada ya kupata viti 29 vya Bunge ambavyo ni sawa na asilimia 51 ya kura.

Hayo yametangazwa na Jaji Mkuu wa Botswana, Terrence Rannowane kufuatia uchaguzi mkuu wa Jumatano iliyopita wa kuwachagua wabunge 57 na wawakilishi wa serikali za mitaa, chaguzi ambazo zitaainisha rais ajaye wa nchi hiyo.

Jaji Mkuu wa Bostwana, Terrence Rannowane amesema mapema leo Ijumaa kwamba: "Japokuwa kura bado zinahesabiwa lakini idadi ya viti vya Bunge vya chama tawala cha BDP vinaniruhusu kumtangaza Mokgweetsi Masisi kama rais mteule wa Botswana."

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi

Chama kikuu cha upinnzani cha Umbrella for Democratic Change (UDC) kimepata viti 13 vya Bunge, Botswana Patriotic Front  kimepata viti 3 na kile cha Alliance for Progressive kimepta kiti kimoja. Matokeo hayo ni ya asilimia 73 ya kura zote za uchaguzi huo zilikuwa tayari zimehesabiwa.

Chama tawala cha BDP sasa kitakuwa na kibarua cha kufanya magezi katika uchumi wa Botswana ambao umekuwa ukistawi kwa asilimia 8 kwa mwaka tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Mwingereza mwaka 1966. Hata hivyo mafanikio hayo yanayoifanya Botswana kuwa miongoni mwa nchi zilizofanikiwa zaidi barani Afrika yanakabiliwa na tishio kubwa kutokana na uchumi wa nchi hiyo kutegemea zao moja tu, yaani madini ya almasi.