Mamia ya raia wa Ethiopia waondoka Saudia Arabia
Serikali ya Ethiopia imewaondoa mamia ya raia wake kutoka Saudi Arabia katika kipindi cha wiki za hivi karibuni.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia Nebiat Getachew amesema katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, serikali ya Ethiopia imewarejesha nyumbani raia 400 wa nchi hiyo waliokuwa Saudi Arabia.
Amesema watu hao waliorejeshwa nyumbani walikuwa wakiishi Saudi Arabia kinyume cha sheria. Aidha amesema Ethiopia inawarejesha nyumbani raia wake waliokuwa wakiishi katika nchi kadhaa za Mashariki ya Kati zikiwemo Lebanon na Yemen.
Idadi kubwa ya raia wa Ethiopia nchini Saudi Arabia na nchi zingine za Kiarabu hulalalmika kuhusu mateso na madhila wanayopata kutoka kwa waajiri wao.
Ili kuwalinda raia wake, serikali ya Ethiopia imetiliana saini mapatano na serikali za Saudia, Imarati na Jordan. Ethiopia inataraji kuwa mapatano hayo yatawezesha raia wake kufanya kazi bila kuteswa au kudhalilishwa katika nchi hizo za Kiarabu hasa Saudi Arabia. Kila mwaka maelfu ya raia wa Ethiopia huingizwa kinyume cha sheria Saudi Arabia na nchi zingine za Kiarabu na kulazimishwa kufanya kazi katika mazingira mabaya sana.