HRW: Tanzania inakiuka sheria kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi kutoka Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56937-hrw_tanzania_inakiuka_sheria_kuwarejesha_kwa_nguvu_wakimbizi_kutoka_burundi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema serikali ya Tanzania imewarejesha kwa nguvu makwao zaidi ya wakimbizi 200 kutoka Burundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2019 00:54 UTC
  • HRW: Tanzania inakiuka sheria kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi kutoka Burundi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema serikali ya Tanzania imewarejesha kwa nguvu makwao zaidi ya wakimbizi 200 kutoka Burundi.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Human Rights Watch imesema mnamo Oktoba 15, Tanzania ilitishia kuwakamata na kuwaweka kizuizini wakimbizi 200 na hivyo wakalazimika kurejea Burundi.

Wakimbizi hao wanalazimishwa kurejea katika nchi yao kufuatia mapatano ya Agosti 24 baina ya serikali za Tanzania na Burundi. Kwa mujibu wa mapatano hayo, ifikapo Disemba 31, wakimbizi 180,000 wa Burundi walioko Tanzania watarejeshwa katika nchi yao watake wasitake. Human Rights Watch imetoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu Afrika iishinikize serikali ya Tazania isitieshe sera yake ya kuwalazimisha wakimbizi kurejea makwao.

Aidha shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeitaka Tume ya Umoja wa Mataifa ya Wakimbizi UNHCR kutosimamia zoezi hilo la kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi.

Mamia ya raia wa Burundi walilazimika kukimbia nchi yao kufuatia ghasia na machafuko yaliyoigubika tangu mwaka 2015 wakati Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu, hatua ambayo ilikuwa kinyume na katiba ya nchi hiyo. Kipindi hicho raia zaidi ya laki nne wa Burundi walikimbilia nchi za nje hasa katika nchi jirani za Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wakimbizi wengi kutoka Burundi wanasema maisha yao yatakuwa hatarini wakirejea makwao.