Oct 31, 2019 07:57 UTC
  • Wanajeshi 12 wa Niger wauawa katika shambulio la Boko Haram

Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa, wanajeshi 12 wa nchi hiyo wameuawa baada ya kambi yao kushambuliwa na kundi la kigaidi la Boko Haram kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema kuwa, shambulio hilo lilitekelezwa jana na watu wasiojulikana ambao wanasadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika mji wa Diffa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Niger wanajeshi wengine wanane wa nchi hiyo wamejeruhiwa katika shambulio hilo la wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi wake mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Bokko Haram

Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na dini ya Uislamu limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi jambo ambalo limepelekea liendelee kutekeleza mashambulizi na mauaji nchini humo na maeneo ya jirani.

Tags