Serikali ya Ethiopia: Watu 78 wameuawa katika maandamano, idadi inaweza kuongezeka
Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa watu wasiopungua 78 waliuawa katika maandamano ya upinzani ya kupinga muamala mbaya dhidi ya mwanaharakati mwenye ushawishi mkubwa, ambaye pia ni mjasiriamali wa vyombo vya habari nchini humo.
Billene Seyoum, msemaji wa Waziri Mkuu wa Ethiopia amewaeleza waandishi wa habari kuwa, watu hao waliouawa, walifariki katika kile alichokiita, "kitendo cha fujo na machafuko yasiyo na maana hata kidogo" yaliyotokea katika mikoa ya Oromia na Harari pamoja na mji wa Dire Dawa ulioko mashariki ya nchi.
Bi Seyoum ameongeza kuwa, watu 409 wamekamatwa katika maandamano hayo yaliyozuka katika mji mkuu Addis Ababa na katika mkoa wa Oromia tarehe 23 Oktoba baada ya mwanaharakati mashuhuri Jawar Mohammed, ambaye pia ni mwasisi wa Mtandao wa Habari wa Oromia kuvituhumu vyombo vya usalama kuwa vinapanga kutekeleza hujuma ya shambulio dhidi yake, madai ambayo Polisi imeyakanusha.
Msemaji wa serikali ya Ethiopia amebainisha kuwa, uchunguzi ungali unaendelea na kwamba idadi ya waliofariki na ya watu watakaotiwa nguvuni inaweza kuongezeka.
Maandamano ya kumuunga mkono Jawar Mohammed yalianza kwa amani Oktoba 22 usiku kwa maelfu ya wafuasi wa mwanaharakati huyo kukusanyika kandokando ya nyumba yake na kufunga njia inayoelekea huko.
Vijana mashababi kutoka kabila lake la Orono ambalo ndilo analotoka pia Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed walielekeza hasira zao kwa kiongozi huyo wakisema amewasaliti kwa kuamiliana vibaya na Mohammed Jawar.
Harakati za Jawar za kuratibu na kuhamasisha maandamano ya mitaani zilisaidia kumweka madarakani Abiy mwaka uliopita.../