Nov 17, 2019 07:39 UTC
  • AU: Jamii ya kimataifa ichangie ustawi wa viwanda Afrika

Umoja wa Afrika umetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuwa na mchango endelevu na amilifu katika ustawi wa viwanda katika nchi za Afrika.

AU yenye nchi wanachama 55 ilitoa mwito huo jana Jumamosi, kwa mnasaba wa kukaribia Wiki ya Viwanda Afrika (African Industrialization Week AIW-2019). 

Mkutano wa Wiki ya Viwanda Afrika unatazamiwa kufanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kuanzia Novemba 18 (kesho Jumatatu) hadi Novemba 22, chini ya kaulimbiu inayosema, "Kunyanyua Sekta ya Viwanda Afrika, ili kufanikisha Makubaliano ya Eneo Huria la Biashara  Afrika (AfCFTA)."

Makubaliano ya AfCFTA yalifikiwa na viongozi wa Afrika katika mkutano uliofanyika mji mkuu wa Niger, Niamey Julai mwaka huu. Nchi za Afrika zinatazamiwa kuanza kufanya biashara chini ya mpango huo kuanzia mwezi Julai mwaka ujao 2020. 

Nembo ya Umoja wa Afrika 

Kwa mujibu wa wachumi, iwapo mpango huo utatekelezwa barabara, uchumi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) unatazamiwa kuimarika na kufikia hadi kiwango cha dola trilioni 3.4.

AU imesema ujumbe wa wataalamu 1000 wa Kiafrika kutoka sekta binafsi, umma, asasi za kiraia, washiriki wa maendeleo, na wanafikra wanatazamiwa kushiriki mkutano huo wa Addis Ababa unaoanza kesho. 

 

Tags