Rwanda: Tunafuatilia kadhia ya kukamatwa mamia ya raia wetu Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57515-rwanda_tunafuatilia_kadhia_ya_kukamatwa_mamia_ya_raia_wetu_uganda
Balozi wa Rwanda jijini Kampala amesema wanafuatilia kwa karibu habari ya kukamatwa mamia ya Wanyarwanda na maafisa usalama wa Uganda, katika mji wa Kisoro, magharibi mwa Uganda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 26, 2019 11:25 UTC
  • Rwanda: Tunafuatilia kadhia ya kukamatwa mamia ya raia wetu Uganda

Balozi wa Rwanda jijini Kampala amesema wanafuatilia kwa karibu habari ya kukamatwa mamia ya Wanyarwanda na maafisa usalama wa Uganda, katika mji wa Kisoro, magharibi mwa Uganda.

Frank Mugambage amesema, "Hatujaarifiwa chochote kuhusu kukamtwa kwa raia hao wa Rwanda namna ambavyo imekuwa ikifanyika huko nyuma, habari hizo tumezipata kupitia kwa vyombo vya habari na tunafuatilia kwa karibu."

Duru za habari zinaarifu kuwa, maafisa usalama wa Uganda jana waliwatia mbaroni Wanyarwanda kati ya 150 hadi 200 na kisha kuwapeleka katika kituo cha polisi cha Kisoro, mpakani mwa nchi hizo mbili.

Inaarifiwa kuwa, mara ya mwisho vyombo vya usalama vya Uganda kukamata idadi kubwa ya Wanyarwanda ilikuwa mwezi Julai mwaka huu, ambapo raia 40 wa nchi hiyo walitiwa nguvuni wakiwa katika kanisa moja jijini Kampala.

Joto la mzozo baina ya Rwanda na Uganda limekuwepo tangu mwanzoni mwa mwaka huu na limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.

Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda jijini Luanda

Hii ni katika hali ambayo, tarehe 21 ya mwezi Agosti mwaka huu, Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda walisaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda yenye lengo la kumaliza uhasama na mzozo uliopo baina ya mataifa hayo mawili jirani.

Baada ya kutiliwa saini makubaliano hayo, Rwanda ilitoa orodha ya raia wake wanaozuiliwa nchini Uganda ambapo Kampala iliahidi kushughulikia majina hayo kupitia mchakato wa kisheria na kuwaachia huru wale ambao hawatapatikana na ushahidi wa kuwatia hatiani.