Jeshi la Kongo DR lasema limeua makumi ya wanamgambo wa ADF
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57668-jeshi_la_kongo_dr_lasema_limeua_makumi_ya_wanamgambo_wa_adf
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuwauwa wanamgambo zaidi ya 80 wa ADF Nalu mjini Beni, mashariki mwa nchi, katika operesheni dhidi ya makundi ya wapiganaji waliojizatiti kwa silaha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 04, 2019 03:50 UTC
  • Jeshi la Kongo DR lasema limeua makumi ya wanamgambo wa ADF

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuwauwa wanamgambo zaidi ya 80 wa ADF Nalu mjini Beni, mashariki mwa nchi, katika operesheni dhidi ya makundi ya wapiganaji waliojizatiti kwa silaha.

Jeshi la DRC lililazimika kuanzisha operesheni hii mashariki mwa Kongo mnamo Oktoba 30, kufuatia mauaji ya watu zaidi ya 100 katika mashambuilizi na hujuma za wanamgambo wa ADF Nalu wanaotokea Uganda.

Wakazi wa Beni na miji mingine ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo wamekuwa wakifanya maandamano ya kutaka askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) waondoke nchini humo kutokana na kushindwa kwao kuwalinda.

Ijumaa iliyopita, wanavijiji wasiopungua 19 waliuliwa kwa umati na wapiganaji wanaoaminika kuwa wa ADF wenye ngome zao ndani ya misitu iliyoko kwenye mpaka wa Uganda.

Wanamgambo wa ADF wanaowahangaisha wakazi wa mashariki mwa DRC

Akthari ya wahanga hao waliuawa kwa kukatwa katwa kwa mapanga au kukatwa vichwa na wapiganaji hao. Tarehe 24 Novemba pia, wakazi wengine wanane wa Beni waliuliwa na waasi hao wa ADF.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu maisha ya raia wakiwemo wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambako machafuko yanazidi kushika kasi.