AFRICOM: Russia ilitungua drone ya Marekani nchini Libya
Jeshi la Marekani limedai kuwa Jeshi la Ulinzi wa Anga la Russia lilitungua drone yake katika mji mkuu wa Libya, Tripoli mwezi uliopita.
Taarifa hiyo imelitaka Jeshi la Russia lirejeshe mabaki ya ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani.
Mnamo Novemba 22, Kamandi ya Jeshi la Marekani Barani Afrika (AFRICOM) ilitangaza kuwa ilipoteza drone yake katika anga ya Tripoli na kudai kuwa ndege hiyo isiyo na rubani 'ilikuwa inatekeleza oparesheni ya kukabiliana na harakati za misimamo mikali.'
Katika taarifa ya leo Jumamosi, Jenerali Stephen Townsend, Mkuu wa AFRICOM amesema anaamini kuwa, walioitungua drone hiyo 'hawakuwa wanajua ni ya Marekani wakati walipoitungua." Amewaambia waandishi habari kuwa, walioitungua drone hiyo sasa wanafahamu ni ya nani na wanakataa kuirejesha.
Mgogoro huo mpya ulianza baada ya kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya, linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, kuanzisha vita vya kila upande mwezi Aprili mwaka huu kwa tamaa ya kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli. Hata hivyo waasi hao wameshindwa kuuteka mji huo licha ya kuungwa mkono kikamilifu na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani.
Libya ilitumbukia katika vita vya ndani tokea mwaka 2011 wakati Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) lilipoteka harakati ya wananchi na kumpindua na kisha kumuua dikteta wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.