Mazungumzo ya Uganda na Rwanda yagonga mwamba
Mkutano wa wajumbe wa Rwanda na Uganda uliofanyika jana Ijumaa jijini Kampala haujakuwa na tija.
Mkutano huo wa jana ulikumbwa na mkwamo baada ya wajumbe wa pande mbili kushindwa kuafikiana kuhusu masuala yenye utata, kama suala la uwepo wa askari wa Uganda nchini Rwanda pamoja na kukamatwa kinyume cha sheria Wanyarwanda nchini Uganda.
Balozi Olivier Nduhungirehe, Waziri wa Masuala ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Rwanda amesema "Tutawashauri marais wa nchi mbili hizi, ili kujua muelekeo na msimamo juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa. Natumai katika siku zijazo, tutakuwa na azma na irada njema ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mzozo uliopo."
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni nchi mbili hizo zilisisitiza umuhimu wa kufungamana na Makubaliano ya Luanda yanayozitaka nchi mbili hizo jirani zijizuie na vitendo vyovyote vya uhasama.
Tarehe 21 ya mwezi wa Agosti mwaka huu, Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda walisaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda yenye lengo la kumaliza uhasama na mzozo uliopo baina ya mataifa hayo mawili jirani.
Joto la mzozo baina ya Rwanda na Uganda limekuwepo tangu mwanzoni mwa mwaka huu na limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.