Dec 15, 2019 07:52 UTC
  • Watu 15 wauawa Nigeria katika shambulizi la Boko Haram

Kwa akali watu 15 wameuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Magumeri, mkoani Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Duru za habari zinaarifu kuwa, shambulizi hilo la kigaidi lilifanyika usiku wa kuamkia leo. Usman Zannah, mbunge katika mkoa huo amesema wanachama wa genge hilo wametekeleza shambulizi hilo kwa kutumia magari 11.

Amesema raia sita na afisa mmoja wa usalama ni miongoni mwa watu waliouawa katika hujuma hiyo ya jana usiku. 

Haya yanajiri masaa machache baada ya kundi hilo la ukufurishaji kuua mateka wanne lililokuwa likiwashikilia, ambao ni wafanyakazi wa shirika la kimataifa la misaada ya kibinaadamu nchini Nigeria.

Ramani inayoonesha mkoa wa Borno wa kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, katika muongo mmoja wa shughuli za kundi la Boko Haram nchini Nigeria, zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamekuwa wakimbizi.

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram lilianzisha shughuli zake za kigaidi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria ambapo hadi sasa limepanua wigo wake hadi katika nchi za Niger, Chad na kaskazini mwa Chad.

Tags