Ethiopia yarusha satalaiti yake ya kwanza katika anga za mbali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57999-ethiopia_yarusha_satalaiti_yake_ya_kwanza_katika_anga_za_mbali
Ethiopia leo Ijumaa imerusha satalaiti yake ya kwanza katika anga za mbali na kujiunga na nchi kadhaa za Kiafrika ambazo zina miradi ya anga za mbali kwa malengo ya ustawi na sayansi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2019 08:13 UTC
  • Ethiopia yarusha satalaiti yake ya kwanza katika anga za mbali

Ethiopia leo Ijumaa imerusha satalaiti yake ya kwanza katika anga za mbali na kujiunga na nchi kadhaa za Kiafrika ambazo zina miradi ya anga za mbali kwa malengo ya ustawi na sayansi.

Maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Ethiopia walikusanyika katika kituo cha Anga za Mbali cha Entoto karibu na mji mkuu Addis Ababa ili kutizama mubashara satalaiti hiyo inayojulikana kwa jina la ETRSS-1, ikirushwa katika anga za mbali kutoka katika kituo kimoja cha kurusha satalaiti nchini China.
Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia, Demeke Mekonnen amezungumza baada ya kushuhudia satalaiti hiyo ikirushwa katika anga za mbali na kusema: "Huu ni msingi wa safari yetu ya kihistoria ya kuelekea katika ustawi."
Solomon Belay, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi ya Anga za Mbali Ethiopia amesema satalaiti hiyo imeundwa kwa ushirikiano wa wahandisi wa China na Ethiopia huku serikali ya China ikichangia dola milioni 6 kati ya milioni saba zilizohitajika kuunda satalaiti hiyo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia akikagua sataliti ya nchi yake iliyokuwa ikiundwa katika kituo cha anga za mbali China mwezi Aprili 2019

Amesema, kutumwa satalaiti hiyo katika anga za mbali kutakuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa usalama wa chakula, ubunifu wa ajira, ustawi wa teknolojia, mamlaka ya kujitawala, kupunguza umasikini na kila kitu ambacho Ethiopia inahitajia kufikia maendeleo endelevu.