Familia zaidi ya 6000 zaathiriwa na mafuriko magharibi mwa Kenya
(last modified Sun, 29 Dec 2019 07:55:56 GMT )
Dec 29, 2019 07:55 UTC
  • Familia zaidi ya 6000 zaathiriwa na mafuriko magharibi mwa Kenya

Afisa wa serikali ya Kenya jana alisema kuwa familia zaidi ya 6000 katika mji wa Kisumu magharibi mwa nchi hiyo zimeathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoanza mapema wiki jana katika mkesha wa Krismasi.

Wakazi wa mji wa Kisumu walioathirika na mafuriko wameeleza kuwa hawana mahali pakavu pa kulala na kwamba wanahofia mafuriko hayo kuongezeka; kwa hiyo wameomba kupatiwa misaada.

Mji wa Kisumu nchini Kenya ulioathiriwa na mafuriko 

Taasisi za serikali kwa upande wake zimesikia kilio cha waathiriwa hao wa mafuriko na kuwataka kuhama makazi yao mara moja na kuelekea katika shule za upili zilizotengwa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko.

Eneo la Afrika Mashariki limekumbwa na mvua nyinyi ambazo si za kawaida zilizosababishwa na ongezeko la joto baharini. Mafuriko, maporomoko ya udongo a kimbunga hadi sasa vimeuwa watu zaidi ya 1200 mashariki na kusini mwa Afrika mwaka huu wa 2019. Hayo ni kwa mujibu wa Taasisi ya Save the Children yenye makao yake nchini Uingereza. 

Wiki jana pia Meya wa mji mkuu wa kibiashara wa Burundi, Bujumbura alitangaza habari ya kuaga dunia watu 15  kutokana na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha huko Bujumbura.