Wahadhari na wanazuoni wa Iran wafanya kikao cha kumuunga mkono Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58261-wahadhari_na_wanazuoni_wa_iran_wafanya_kikao_cha_kumuunga_mkono_sheikh_zakzaky
Wanazuoni wa Kiislamu, maprofesa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamefanya kikao cha kuonyesha uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2020 09:47 UTC
  • Wahadhari na wanazuoni wa Iran wafanya kikao cha kumuunga mkono Sheikh Zakzaky

Wanazuoni wa Kiislamu, maprofesa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamefanya kikao cha kuonyesha uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Kikao hicho ambacho kilifanyika jana Jumatano katika Hauza ya Kidini ya Imam Reza (AS) katika mkoa wa Tehran kilihudhuriwa pia na mabinti watatu wa mwanaharakati huyo wa Kiislamu wa Nigeria, ambaye anaendelea kushikiliwa katika mazingira magumu na vyombo vya usalama vya Nigeria licha ya hali yake mbaya ya afya.

Wasomi hao wa kidini na wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Iran wameendelea kutoa mwito wa kuachiwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe, sambamba na kupewa matibabu ya haraka.

Vikao, marasimu na maandamano yamekuwa yakifanyika hapa nchini Iran kwa ajili ya kushikinikiza kuachiwa huru msomi na mwanaharakati huyo wa Kiislamu wa Nigeria.

Mabinti wa Sheikh Zakzaky katika kikao cha wasomi wa Iran mjini Tehran

Hapo jana pia, mamia ya wanachuo nchini Nigeria waliandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja wakitangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, ambapo walisikika wakipiga nara za kulaani kuendelea kushikiliwa msomi huyo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussaynia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.