'Al-Shabaab' yateka basi na kuua abiria kaunti ya Lamu, Kenya
Kwa akali watu watatu wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kuteka nyara basi la abiria katika kaunti ya Lamu, pwani ya Kenya.
Irungu Macharia, Kamishna wa Kaunti ya Lamu amethibitisha kutokea shambulizi hilo na kubainisha kuwa, basi hilo la abiria lilikuwa linatokea mjini Mombasa likielekea Lamu kabla ya shambulizi hilo.
Inaarifiwa kuwa, watuhumiwa wa kundi la al-Shabaab wamefanya shambulizi hilo la kushtukiza katika eneo la Nyongoro lililoko karibu na wilaya ya Witu, kaunti ya Lamu.
Mapema mwezi uliopita, watu 10 waliuawa katika shambulizi jngine dhidi ya basi la abiria lililofanywa na genge la kigaidi na kitakfiri al-Shabaab katika kaunti ya Wajir, kaskazini mashariki mwa Kenya mpakani na Somalia.
Miaka mitano iliyopita, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao makuu yake nchini Somalia lilifanya hujuma nyingine dhidi ya basi la wasafiri, na kuua 28 miongoni mwao.
Katika akthari ya hujuma hizo za a-Shabaab dhidi ya mabasi ya uchukuzi wa umma, magaidi hao wakufurishaji wanaoua Waislamu wenzao nchini Somalia wamekuwa wakiwalenga tu wasiokuwa Waislamu, kwa shabaha ya kupanda mbegu za chuki na kuwagawa wananchi katika misingi ya dini.