Jan 17, 2020 07:31 UTC
  • Watu 14 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Mali

Umoja wa Mataifa umesema watu 14 kutoka jamii ya Fulani katikati mwa Mali wameuawa katika kile kinachoaminika ni mapigano ya kikabila.

Mashuhuda wanasema, watu waliotekeleza mashambulizi hayo ya jana katika kijiji cha Siba walitumia zana za kale kama mikuki na mishale kutekeleza ukatili huo, ambapo pia waliteketeza kwa moto nyumba za wakazi wa kijiji hicho. Aidha wavamizi hao waliiba mifugo ya watu wa kabila la Fulani.

Baadhi ya duru nchini humo zimeripoti kwamba watu hao wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyowahusisha watu wa kabila la Dogon, ambao ni wawindaji na mahasimu wao wa kabila la Fulani ambao ni wafugaji. 

Mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2019, Jeshi la Mali lilitangaza kuwa limewauwa magaidi 19 katika oparesheni zake mbili katikati mwa nchi hiyo waliohusika na shambulizi dhidi ya jamii ya Waislamu wa kabila la Fulani ambapo waliwaua wanavijiji wawili. 

Wafugaji wa kabila la Fulani katika mkoa wa Mopti katikati ya Mali

Mwezi Oktoba mwaka jana pia wanajeshi 25 wa Mali waliuawa katika shambulio la magaidi wenye silaha. Kundi lenye misimamo ya kufurutu ada lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida kwa jina la AKIM lilitangaza kuhusika na shambulio hilo. 

Maeneo ya kaskazini na katikati mwa Mali yamekumbwa na hali ya mchafukoge tangu mwaka 2012; na kumejitokeza makundi mbalimbali ya wanamgambo wenye silaha na yale yenye kufurutu ada ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi wa maeneo hayo.

Tags