Chama tawala nchini Burundi chamteua mgombea wa urais
Chama tawala cha CNDD-FDD nchini Burundi kimemteua Katibu Mkuu wa chama hicho, Evariste Ndayishimiye kuwa mgombea wa kiti cha urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu.
Ndayishimiye mwenye umri wa miaka 52 mbali na kuwa Katibu Mkuu wa CNDD-FDD, ni Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kijeshi katika Ofisi ya Rais. Aidha amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Burundi.
Tangazo hilo la chama tawala nchini Burundi limekuja wiki chache baada ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kutangaza kwa mara nyingine tena kuwa, hatagombea kiti cha urais katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika Mei 20 mwaka huu.
Kulikuwa na wasi wasi kuwa Nkurunziza ambaye ameiongoza Burundi tangu mwaka 2005 angewania tena kiti hicho, kwa kuzingatia kuwa katiba mpya aliyoiidhinisha inampa kibali cha kusalia madarakani hadi mwaka 2034.
Burundi ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi duniani ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa mapema mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwa atagombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu; hatua ambayo wapinzani walisema ilikuwa kinyume na katiba ya nchi hiyo.