Makumi ya watu wauawa katika mapigano baina ya makundi hasimu CAR
Mapigano makali yaliyotokea baina ya makundi hasimu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yamesababisha mauaji ya makumi ya watu na kuwalazimisha mamia ya wengine kukimbia nyumba zao.
Mauaji haya yametajwa kuwa ndiyo mabaya zaidi kutokea CAR tangu mwezi Februari mwaka jana wakati makundi hasimu nchini humo yaliposaini makubaliano ya amani. Makubaliano hayo yalilenga kukomesha mapigano na kuimarisha amani katika nchi hiyo iliyotumbukia kwenye mapigano ya ndani baada ya wapiganji wa kundi la Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé.
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA kimeripoti kuwa, mapigano ya sasa yametokea katika mji wa mashariki mwa CAR wa Bria baina ya makundi ya kikabila ndani ya Seleka.
Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Antoine Mbao Bogo amesema watu 41 wameuawa katia mapigano hayo. Hata hivyo mkuu wa eneo la Bria, Evariste Binguinendji amesema idadi ya watu waliouawa inafikia 50 na kwamba baadhi ya familia zimezika maiti za jamaa zao mapema, suala ambalo limetatiza zoezi la kujua idadi halisi ya wahanga wa machafuko hayo.
Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Vladimir Monteiro amesema hali ya mambo katika mji wa Bria ni shwari hususan baada ya askari wa kikosi hicho kutumwa eneo hilo kwa ajili ya kutuliza ghasia.
Watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao na wengine milioni 2.7, au nusu ya watu wote CAR wanahitaji msaada kutokana na machafuko na mapigano ya ndani.