Feb 09, 2020 03:29 UTC
  • Watu wasiopungua 11 wauawa katika shambulio la kigaidi Niger

Raia wasiopungua 11 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti huko Niger. Katika shambulio moja lililofanywa juzi Ijumaa wanamgambo wa kundi la kitakfiri na kigaidi la Boko Haram waliwauwa raia sita katika wilaya ya Bosso kusini mashariki mwa mkoa wa Diffa unaopakana na Chad na Nigeria.

Watu wanne wa familia moja nimiongo mwa raia hao waliouliwa na Boko Haram. Maafisa katika wilaya ya Bosso wamethibitisha kujiri shambulio hilo hata hivyo wamesema kuwa watu watano waliuawa wilayani humo.

Katika shambulio la pili lililofanywa na wanamgambo wa kigaidi wa Boko Haram katika mkoa wa Tillaberi unaopakana na Mali; watu wanne waliokuwa na silaha wakiwa kwenye pikipiki mbili waliwafyatulia risasi wafanyakazi katika kijiji cha Molia na kuwauwa wanne miongoni mwao. Shambulio hilo lilifanywa Alhamisi iliyopita. Itakumbukwa kuwa utumiaji wa pikipiki umepigwa marufuku katika eneo hilo huko Niger.

Mikoa ya  Diffa na Tillaberi imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na magaidi wa kitakfiri wenye makao yao kaskazini mwa Nigeria. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa mashambulizi matatu yaliyofanywa mwezi Disemba na Januari ambayo kundi la Daesh lilidai kuhusika yalisababisha vifo vya wanajeshi 174.  

 

 

 

 

 

Tags