Waafrika milioni 239 wanakabiliwa na njaa, utapiamlo
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa FAO Marina Helena Semedo amesema watu takriban milioni 239 wa Afrika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara wanakabiliwa na tatizo la njaa na utapiamlo.
Afisa huyo wa FAO amesisitiza kuwa njia pekee ya kutokomeza kabisa masaibu hayo ni kupitia amani na usalama wa kudumu barani Afrika.
Bi Semedo amebainisha kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa yameweka shabaha kadha muhimu ikiwemo ya kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya Waafrika walio kusini mwa sahara ambao wanaishi katika hali ya umasikini, njaa, na utapiamlo, kwa kuwawezesha kwenye kilimo kinachoungwa mkono ili kusukuma mbele juhudi za nchi kufikia ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030.
Mbali na hayo Bi Semedo pia amesititiza kuwa FAO hivi sasa inatekeleza shughuli mbalimbali za kuongeza mapato kwa ajili ya watu wa vijijini walio masikini.
Kamishna wa Kilimo katika Umoja wa Afrika Josefa Sacko amesema kuna haja ya kuwasilishwa mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za njaa na umasikini barani Afrika. Amesema wakati umefika kukiri kuwa mbinu zinzotumika sasa haziwezi kuzaa matunda. Amesisitiza kuwa kumaliza migogoro Afrika ni muhimu ili kudhamini usalama wa chakula katika bara hilo.