António Guterres ataka kuhitimishwa mapigano ya silaha barani Afrika
António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa kuhitimishwa mapigano ya silaha barani Afrika, ni moja ya masuala muhimu na ya msingi katika kulindwa haki za binaadamu.
Guterres aliyasema hayo Jumapili ya jana katika kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia ambapo akiashiria masuala ya kisiasa nchini Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Somalia, Libya na maeneo ya Sahel, amesisitizia ulazima wa kutatuliwa masuala ya pande hasimu katika nchi hizo na maeneo mengine ya bara hilo kupitia mazungumzo na kuzingatiwa sheria za kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa UN inalipa umuhimu mkubwa suala la kudhaminiwa mishahara ya askari wa kusimamia amani barani Afrika.
Katika sehemu nyingine António Guterres amesisitiza ushirikiano wa kistratijia kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika hususan katika fremu ya makubaliano muhimu kati ya taasisi hizo mbili kwenye kutatua migogoro ya kiusalama na kijamii. Kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika, kilianza shughuli zake jana Jumapili katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia na kitaendelea hadi leo Jumatatu.