Feb 10, 2020 08:21 UTC
  • Uchunguzi: Al Sisi anawaua wapinzani wake kwa

Uchunguzi uliofanywa na televisheni ya al Jazeera ya Qatar umefichua takwimu za kutisha kuhusu idadi ya wafungwa wa kisiasa waliouawa au kuaga dunia kutokana na kutelekezwa, kutopatiwa matibabu kwa makusudi na mazingira mabaya kupita kiasi ndani ya jela za Misri tangu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi mwezi julai mwaka 2013.

Uchunguzi huo uliorushwa hewani jana na televisheni ya al Jazeera umetegemea ushahidi wa wafungwa walioko katika jela za Abdel Fattah al Sisi walioeleza mazingira ya kutisha ndani ya jela hizo ambako makumi ya watu wanafungwa katika seli ya watu 6.

Wafungwa hao wanaeleza kuwa, serikali inawanyika kwa makusudi huduma za tiba na maji safi ya kunywa na kwamba hawapewi chakula cha kutosha au kuruhusiwa kuota jua, suala linalowasababishia wengi miongoni mwao maradhi ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kifua kikuu.

Vilevile wazazi, wake na jamaa wa wafungwa hao wa kisiasa wanasema Idara ya Magereza ya Misri imewazuia wafungwa hao kupata dawa kutoka nje ya jela na kwamba wengi wameaga dunia kutoka na kutelekezwa na vyombo vya dola.

Ripoti ya uchunguzi wa al Jazeera inasema maradhi yaliyozagaa zaidi katika jela za wafungwa wa kisiasa nchini Misri ni pamoja na figo, macho, kiharusi, kisukari na kadhalika. Imenukuu maoni ya wanasheria wanaosisitizia kuwa, jela hizo zimetayarishwa kwa ajili ya kuwaua kimyakimya wanasiasa wanaopinga utawala wa Abdel Fattah al Sisi.

Ripoti hiyo imesema kuwa, kuanzia mwezi julai 2013 hadi mwaka 2019 wafungwa 958 wameaga dunia katika jela za Misri wakiwemo 677 walioaga dunia kutokana na kunyimwa matibabu, 136 waliofariki dunia kutokana na mateso na 65 wamejingonya kutokana na sulubu walizokuwa wakikabiliana nazo katika jela za Misri.

Ripoti hiyo imesema kuwa miongoni mwa wafungwa wa kisiasa walioaga dunia katika jela za Misri kutokana na kunyimwa huduma ya matibabu ni Rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Morsi.    

Tags