Ramaphosa: Mapendekezo ya Muamala wa Karne yanafanana na ya 'apartheid'
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema mapendekezo ya Rais Donald Trump kwenye 'Muamala wa Karne' yanashabihiana na mfumo wa kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Ramaphosa ambaye jana Jumapili alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika ameuambia umoja huo kuwa, "Nikisikiliza na kusoma yote yaliyosemwa na kuandikwa kuhusu mapendekezo hayo, fikra zangu zinarejea nyuma kwenye kumbukumbu za historia mbaya ambayo wananchi wa Afrika Kusini walipitia katika kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) miaka ya 90."
Naye Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ambaye ni mwenyekiti anayeondoka wa AU amesema katika hotuba yake mbele ya umoja huo kuwa, kadhia ya Palestina itasalia katika nyoyo na fikra za wananchi wa Afrika.
Hapo jana pia, Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alisema kuwa, mpango wa Muamala wa Karne uko dhidi ya Wapalestina na unakinzana na sheria za kimataifa.
Rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel walizindua mpango huo wa kibaguzi walioupa jina la 'Muamala wa Karne' tarehe 28 Januari mwaka huu. Hata hivyo mpango huo umeendelea kupingwa katika kila pembe ya dunia.