Amnesty yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya waandishi wa habari nchini Somalia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa anga ya machafuko na ukatili inayotawala nchini Somalia inawafanya waandishi habari waishi katika hali ya woga na wahka.
Amnesty International imesema kuwa, waandishi habari wasiopungua 8 wameuawa nchini Somalia tangu Mohamed Abdullahi Farmajo aliposhika madaraka ya nchi mwaka 2017 na wengine wamenusurika majaribio ya kuuliwa au wametiwa nguvuni na kulazimishwa kuchucha habari zao.
Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Amnesty International kanda ya mashariki mwa Afrika imesema kuwa, waandishi wa habari nchini Somalia wanazingirwa na wanakabiliana na hatari kama za kulengwa kwa milipuko ya mabomu ya kutengwa ndani ya magari, kulengwa kwa risasi, kupigwa au kutiwa nguvuni kiholela.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeituhumu serikali ya Somalia kuwa haifanyi uchunguzi kuhusu mashambulizi yanayowalenga waandishi habari na kwamba inachuja ripoti zote zinazokosoa utendaji wa serikali.
Mapigano ya ndani na mashambulizi yanayoendele kufanywa na kundi la kigaidi la al Shabab katika maeneo mbalimbali ya Somalia yamezidisha ukosefu wa amani katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika.