Lassa yaingia Lagos, idadi ya waliokufa kwa homa hiyo Nigeria yapindikua 100
Kesi ya kwanza ya mlipuko wa homa ya Lassa imethibitishwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria, Lagos huku idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini humo ikiongezeka.
Jana Alkhamisi serikali ya jimbo la Lagos iliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter ikisema kuwa, "mtu aliyeathiriwa ametengwa katika chumba mahsusi hospitalini. Watu 63 wanaoshukiwa kuwa walitangamana na muathiriwa huyo na huenda pia wamembukizwa wanafuatiliwa."
Kuthibitishwa kwa kesi ya homa ya Lassa Lagos kumeibua hofu haswa kwa kuzingatia kuwa, mji huo wa kibiashara wenye watu milioni 20 una msongamano na shughuli nyingi.
Kituo cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza nchini Nigeria (NCDC) kimeripoti kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha nchini humo kutokana na mlipuko mpya homa ya Lassa imeongezeka na kufikia 103.
Mwaka mmoja uliopita, serikali ya Nigeria ilitangaza kuzuka ugonjwa wa homa ya Lassa nchini humo ambapo katika kipindi cha mwaka uliopita wa 2019 karibu watu 170 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa homa ya Lassa ulishuhudiwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1969 katika mji wa Lassa na kwa sababu hiyo ulipewa jina la mji huo. Ugonjwa huo unashabihiana sana na ule wa Ebola na Marbug.