Makumi ya waandamanaji wajeruhiwa katika maandamano nchini Ethiopia
Maafisa wa jeshi la polisi la Ethiopia wametangaza kuwa, makumi ya watu wamejeruhiwa baada ya kutokea mripuko wa bomu katika maandamano ya kumuunga mkono Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Polisi wa eneo la Oromia wametangaza kuwa, bomu hilo lililokuwa limetegwa katika njia yalipokuwa yanapita maandamano ya kumuunga mkono Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed limejeruhi watu 31. Mripuko huo umetokea katika mji wa Ambo ulioko umbali wa kilomita 100 kutoka Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.
Maafisa wa polisi wamesema kuwa, watu 6 wameshatiwa mbaroni hadi hivi sasa kutokana na kuhusishwa na mripuko huo.
Maafisa hao wa polisi wamesema kuwa, waasi wa Oromo ambao ni kundi la kijeshi lililojitenga na harakati ya ukombozi ya Oromo ndiyo iliyohusika na utegaji bomu huo.
Hivi sasa Ethiopia inajiandaa kufanya uchaguzi wa nchi nzima wa Bunge. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu wa 2020, hata hivyo kampeni za uchaguzi zitaanza mwanzoni mwa mwezi Mei.
Machafuko katika eneo la Oromia la katika mwa Ethiopia yalianza mwaka 2016 na baadaye kuenea hadi kaskazini mwa nchi hiyo. Mashirika ya haki za binadamu yalitangaza kuwa mamia ya watu waliuawa katika machafuko hayo.
Inafaa kusema hapa kwamba, maandamano ya kupinga serikali katika mkoa wa Oromia yamebadilika na kuwa machafuko ya kikabila na kupelekea watu wengi kuuawa na kujeruhiwa.