Umoja wa Mataifa wakaribisha kusainiwa makubaliano ya amani Kongo DR
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amepongeza hatua ya kusainiwa makubaliano ya amani baina ya makundi ya waasi na serikali ya DRC.
Duru za habari zinaarifu kuwa, mwakilishi huyo wa UN katika masuala ya Kongo DR ameeleza matumaini yake kuwa serikali itafikia makubaliano ya amani na makundi mengine ya waasi wanaobeba silaha katika mkoa wa Ituri mashariki mwa nchi kama ilivyofanya na makundi ya "Mai Mai" na "Free Congo Patriotic Alliance."
Habari zaidi zinasema kuwa, makundi ya waasi yaliyosaini mapatano hayo yameitaka serikali kuu ya DRC iwaachie huru wapiganaji wao inaowazuilia, huku yakiahidi kuwaachia huru pia askari wa serikali.
Aidha pande mbili hizo zimeafikiana kushirikiana na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya amani ya nchi hiyo, sambamba na kumaliza mgogoro na mchafuko yanayoshuhudiwa nchini humo kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
Makubaliano hayo amani baina ya makundi ya waasi na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalisainiwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi, chini ya usimamizi wa wabunge wa mkoa huo.
Maeneo ya katikati, mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC yanashuhudia mapigano na vita kwa zaidi ya miaka 20 sasa, licha ya uwepo wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.