Mtawala wa Misri El Sisi aendelea kukiuka haki za binadamu
(last modified Thu, 28 Apr 2016 07:49:08 GMT )
Apr 28, 2016 07:49 UTC
  • Mtawala wa Misri El Sisi aendelea kukiuka haki za binadamu

Rais Abdel Fatah el Sisi nchini Misri ameendelea kukiuka haki za binaadamu huku akikosolewa kitaifa na kimataifa kutokana na kuendelea kuzorota hali ya mambo nchini humo.

Katika kuendelea ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Misri, mwendesha mashtaka nchini humo mnamo Jumatano Tarehe 27 Aprili alitangaza kuendelea kushikiliwa korokoroni wanaharakati watatu wa kisiasa kwa tuhuma za kushiriki katika maandamano kinyume cha sheria.

Katika upande mwingine watu takribani 400 wanaripotiwa kukamatwa siku ya Jumatatu katika maandamano makubwa yaliyoitishwa kupinga hatua ya serikali ya Misri kuipatia Saudia umiliki wa visiwa viwili vya Bahari ya Sham vya Tiran na Sanafir.

Duru ya mpya ya maandamano dhidi ya serikali ya El Sisi yalianza baada ya safari ya Mfalme Salman wa Saudia nchini humo ambapo alikabidhiwa rasmi visiwa hivyo ambavyo ni milki ya Misri.

Katika kuendeleza ukandamizaji, Rais El Sisi na waziri wake wa mambo ya ndani Majdi Abdul Ghaffar wamewaonya waandamanaji kuwa watachukuliwa hatua kali.

Wananchi wa Misri wamepuuza onyo hilo la serikali na kujitokeza kwa wingi mitaani kuandamana huku wakimtaka El Sisi aondoke madarakani.

Katika makabiliano ya hivi karibuni ya vikosi vya usalama na waandamanaji, waandamanaji wawili wanaripotiwa kuuawa na wengine karibu 400 kutiwa mbaroni.

Serikali ya Misri inatumia sheria iliyowekwa kuwakandamiza waandamanaji. Kwa mujibu wa sheria hiyo, maandamano yasiyo na idhini ya Wizara ya Mambo ya Ndani yanachukuliwa kuwa ni maandamano haramu na wanaokiuka sheria hiyo wanahukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani. Ukandamizaji huo wa Misri unazidi kulaaniwa kitaifa na kimataifa.

Jumuiya ya Waandishi Habari Misri imebainisha wasiwasi wake kufuatia kutiwa mbaroni waandishi kadhaa wa habari katika matukio ya Aprili 25 na imesema itawasilisha malalamiko dhidi ya waziri wa mambo ya ndani.

Ukandamizaji dhidi ya waandishi habari unakumbusha zama za utawala wa kiimla wa dikteta aliyetimuliwa madarakani Husni Mubarak.

Magdalena Mughrabi mwakilishi wa shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International eneo la Afrika Kaskazini alisema juzi Aprili 26 kuwa, kuna ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu Misri. Amewalaumu watawala wa Misri kuwa wanakandamiza maandamano kwa mabavu.

Mwaka jana katika maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa kutwaa madaraka El Sisi, vyombo vya habari vya Misri na vya kimataifa vilitaja ukiukwaji wa haki za binaadamu kama sifa ya kipekee ya serikali ya El Sisi.

Sera ya seirkali ya El Sisi ,anayepata himaya kamili ya jeshi, ni kukandamiza kila aina ya maandamano dhidi ya serikali na kuibua hali ya hofu na wahka ndani ya nchi hiyo.

Ingawa hadi sasa kumeshuhudiwa kupungua maandamano Misri kutokana na mkono wa chuma unatoumiwa, lakini hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuitunuku Saudia visiwa viwili muhimu mkabala wa kupokea mabilioni ya dola ni jambo ambalo limewakasirisha sana Wamisri. Hatua hiyo ya kupeana ardhi ya nchi iyo imepelekea Wamisri kutangaza wazi upinzani wao kwa serikali na natija ya hilo ni kuendelea kukiukwa haki za binadamu.

Tags