Tanzania yathibitisha kuwepo mgonjwa wa corona nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59783-tanzania_yathibitisha_kuwepo_mgonjwa_wa_corona_nchini_humo
Serikali ya Tanzania imetangaza kuwepo mgonjwa wa COVID-19 maarufu kama virusi vya corona ambaye aliingia nchini humo jana Jumapili.
(last modified 2025-11-15T16:53:52+00:00 )
Mar 16, 2020 14:21 UTC
  • Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Tanzania
    Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Tanzania

Serikali ya Tanzania imetangaza kuwepo mgonjwa wa COVID-19 maarufu kama virusi vya corona ambaye aliingia nchini humo jana Jumapili.

Akizungumza na waandishi habari leo mjini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa tarehe 15 Machi 2020, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, walipokea msafiri raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 46 ambaye aliwasili na ndege ya Rwanda kutokea Ubelgiji. Mgonjwa huyo ambaye ni mwanamke alifanyiwa ukaguzi uwanjani hapo na kuonekana kutokuwa na homa lakini baadae alianza kujisikia vibaya akiwa hotelini na kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mt. Meru na baada ya kupimwa amethibitishwa kuwa ana maambukizi ya ugongjwa wa corona.

Waziri Ummy amewahakikishia Watanzania kuwa serikali imejiandaa vyema kukabiliana na ugonjwa huo huku akiwataka watu kuendelea kuchukua tahadhari zaidi.

Aidha serikali inashirikiana na Shirika la Afya Duniani-WHO na wadau katika kuendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huu.

Raia wametakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kadri wanavyopokea taarifa na elimu za mara kwa mara kwa njia mbalimbali.

Halikadhalika amewataka Watanzania wasiokuwa na safari za lazima kusitisha safari zao kwenye nchi zenye maambukizi.

Pia amewataka Watanzania kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kubusu, kuepuka kushika pua, mdomo na macho.