Iran iko tayari kuisaidia Marekani kudhibiti ugonjwa wa Covid-19
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59864-iran_iko_tayari_kuisaidia_marekani_kudhibiti_ugonjwa_wa_covid_19
Naibu Waziri wa Afya wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuisaidia Marekani kudhibiti mripuko wa ugonjwa wa COVID-19, kutokana na udhaifu wa mfumo wa afya wa nchi hiyo ambao umeshindwa kuzuia wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 20, 2020 10:01 UTC
  • Iran iko tayari kuisaidia Marekani kudhibiti ugonjwa wa Covid-19

Naibu Waziri wa Afya wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuisaidia Marekani kudhibiti mripuko wa ugonjwa wa COVID-19, kutokana na udhaifu wa mfumo wa afya wa nchi hiyo ambao umeshindwa kuzuia wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona nchini humo.

Ali-Reza Raeisi amewaambia waandishi wa habari kuwa, "mfumo wa afya wa Marekani hauwezi kudhibiti janga la maambukizi ya kirusi cha corona yanayoenea kwa kasi, hivyo Iran ipo tayari kuisaidia nchi hiyo kudhibiti ugonjwa huo."

Amesisitiza kuwa, kwa vile ni nchi ya Kiislamu, Iran haifurahii kuona udhaifu huo wa mfumo wa afya wa Marekani hivyo iko tayari kuipa nchi hiyo uzoefu wake katika kudhibiti ugonjwa wa Covid-19.

Naibu Waziri wa Afya wa Iran ameeleza bayana kuwa, kama kuna sehemu ambako taarifa na habari za janga hili (la corona) zimefichwa na kufunikwa, basi ni Marekani.

Katika hali ambayo majimbo yote 50 ya Marekani yamekumbwa na kirusi cha corona, lakini takwimu za serikali ya Washington zinadai kuwa eti walioaga dunia kwa ugonjwa huo kufikia sasa ni watu 200 tu. 

Madaktari na wauguzi wa Iran wakiwa kazini

Ameeleza kusikitishwa kwake na ukiritimba wa utawala wa Donald Trump katika kutoa taarifa za maambukizi ya kirusi cha corona nchini humo, katik hali ambayo taarifa za mripuko wa ugonjwa huo nchini Iran ziko wazi sana hata zinawekwa katika tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya watu wote kuziona.

Huku hayo yakiarifiwa, Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu nchini Iran imetangaza kwamba, hadi sasa watu 6,745 walioathirika na kirusi cha corona hapa nchini wamepona,  na kwamba jumla ya watu 117,631 wameathiriwa na kirusi hicho, na 1,135 miongoni mwao wamepoteza maisha kwa maradhi hayo.