Mfungwa wa tatu wa kisiasa afia jela akiteswa nchini Misri
Jumuiya za kutetea haki za binadamu nchini Misri zimatangaza kuwa, mfungwa mwingine wa kisiasa amefia jela akiwa chini ya mateso ya maafisa usalama wa nchi hiyo.
Jumuiya hizo zimeripoti kuwa, mfungwa huyo wa kisiasa ameaga dunia wakati alipokuwa akipewa mateso ndani ya makao makuu ya Shirika la Usalama wa Taifa la Misri katika mji wa Shibin El Kom makao makuu ya mkoa wa Monufia. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, idadi ya wafungwa wa kisiasa waliofia mahabusu nchini Misri tangu Alkhamisi iliyopita imefikia watu watatu.
Taasisi ya Haki na Uhuru ya Misri imetangaza kwamba: Muhandisi Hisham Abu Ali ameaga dunia akiwa chini ya mateso ndani ya makao ya Shirika la Usalama wa Taifa katika mji wa Shibin El Kom mkoani Monufia."
Taasisi hiyo imesema Abu Ali alikuwa miongoni mwa wanaharakati wa kisiasa wenye ushawishi mkubwa nchini Misri na kuongeza kuwa, alitoweka kwa kipindi cha wiki mbili na baadaye akaachiwa huru kisha akakamatwa tena na Shirika la Usalama wa Taifa.
Familia ya mwanaharakati huyo wa kisiasa imesema maafisa wa Shirika la Usalama wa Taifa wamewapigia simu wakiwataka kwenda kuchukua maiti yake. Familia hiyo imesisitiza kuwa kabla ya kutiwa nguvuni, Abu Ali alikuwa mzima na mwenye afya nzuri na alikuwa hasumbuliwi na maradhi ya aina yoyote.
Subhi Fathi Abdel-Samad Ramadan maarufu kwa jila la Sobhi al Banna na Hamdi Abduh Hashim Abdel Barr ni wafugwa wengine wa kisiasa walioaga dunia wakiwa mahabusu siku ya Alkhamisi iliyopita.
Maelfu ya wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa mahabusu na gerezani nchini Misri wanasumbuliwa na mateso, kutelekezwa na kunyimwa huduma za matibabu. Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa jela na mahabusu za Msri zimegeuka na kuwa kama makaburi ya umati tangu baada ya mapinduzi ya Juni mwaka 2013 yaliyomuondoa madarakani rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia, Muhammad Morsi.