Mar 24, 2020 14:44 UTC
  • Shambulio la kigaidi laua wanajeshi 70 kaskazini mwa Nigeria

Askari wasiopungua 70 wa jeshi la Nigeria wameuawa katika shambulio la kigaidi lililotokea katika jimbo la Borno kaskazini mwa nchi hiyo.

Duru za usalama za Nigeria zimetangaza leo kuwa, magaidi walishambulia kwa bunduki aina ya RPG lori lililokuwa limebeba wanajeshi karibu na kijiji cha Gorji katika jimbo la Borno.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa usalama, katika shambulio hilo ambalo lilifanywa hapo jana, lori hilo lilishika moto na watu wote waliokuwemo ndani yake, ambao wanakadiriwa kuwa ni zaidi ya askari 70, waliuawa.

Afisa huyo ameongeza kuwa: Askari wengine kadhaa walijeruhiwa katika shambulio hilo na baadhi ya wengine walikamatwa mateka na magaidi hao.

Askari wa jeshi la Nigeria

Lori hilo la kijeshi lililoshambuliwa, lilikuwa linaelekea kwenye kambi moja inayodhibitiwa na tawi la kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) magharibi mwa Afrika kwa lengo la kufanya shambulio dhidi ya kambi hiyo.

Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la Jumatatu.

Karibu siku 10 zilizopita pia watu wasiopungua 15 waliuawa na majengo zaidi 50 yalibomolewa katika mripuko uliotokea kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria, Lagos.../

Tags