Afisa mmoja wa ubalozi wa Marekani ashambuliwa kwa risasi mjini Khartoum Sudan
Ubalozi wa Marekani nchini Sudan umetangaza kuwa, afisa mmoja wa ubalozi huo amesalimika kifo baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Kharotum.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, duru moja wa ubalozi wa Marekani mjini Khartoum imethibitisha habari hiyo na kufafanua kwamba, afisa mmoja wa ubalozi wa Marekani jana Alkhamisi alishambuliwa kwa risasi na mtu asiyejulikana lakini amenusurika kifo.
Duru hiyo imeongeza kuwa, mwanadiplomasia huyo wa Marekani ameshambuliwa wakati akiwa anaendesha gari kurejea nyumbani kutoka eneo lake la kazi na kwamba kioo cha mbele cha gari yake kilisambaratishwa kwa risasi, akashindwa kudhibiti usukani na hivyo gari yake kugonga magari mengine kadhaa.
Ikumbukwe kuwa Sudan ni moja ya nchi zilizoko kwenye orodha ya Marekani ya nchi ilizoziwekea vikwazo kwa madai ya kuunga mkono ugaidi.
Vyama na wananchi wa Sudan mara kwa marsa wamekuwa wakidhihirisha hasira zao dhidi ya siasa hizo za kibeberu za Marekani.
Wananchi wa Sudan wanaamini kuwa, viongozi wa Marekani wameahidi kwa maneno tu kuitoa nchi hiyo katika orodha ya nchi inazodai zinaunga mkono ugaidi. Wanasema lengo hasa la Marekani ni kuzidi kuishinikiza Sudan ili ipigie magoti siasa za kibeberu za Washington na iwaruhusu viongozi wa Marekani waendelee kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.